Kama
tunavyofahamu, nchi yetu ina aina mbalimbali za nyoka ambao pindi
wakimuuma mtu huleta madhara mbalimbali ya kiafya. Aidha tunafahamu
kwamba tatizo hili lipo zaidi katika maeneo ya vijijini ambako uwezo wa
wananchi kumudu gharama za matibabu ni mdogo.
Dawa za kutibu
sumu ya nyoka huagizwa kutoka nje ya nchi. Dawa hizo siyo tu
hazipatikani kwa urahisi, bali pia zinapatikana kwa gharama kubwa. Bei
ya kununulia dawa hizi ni kati ya dola za kimarekani 55 hadi 85 (yaani
shilingi za kiTanzania 118,250 hadi 182,750) kwa kichupa kidogo (vial)
kimoja. Kichupa hicho huweza kutumika kwa wagonjwa wanne, lakini mara tu
baada ya kufunguliwa dawa hiyo huwa haifai tena kutumika ndani ya mwezi
mmoja tu.
Pamoja na
changamoto hizo, Serikali kupitia MSD kila mwaka huagiza dawa hizi kwa
ajili ya mahitaji hayo ya kutibu wagonjwa walioumwa na nyoka, ambapo bei
ya kuinunua kutoka MSD ni TZS 200,000/= kwa kichupa kimoja. Hospitali
zetu mbalimbali zimekuwa zikiagiza dawa hizi kutoka MSD na kwa washitiri
wengine kwa bei hii au zaidi na kuwatibu waathirika wanaohitaji dawa za
sumu za nyoka mara zinapohitajika.
Napenda
kuwakumbusha kwamba kwa mujibu wa Sera ya Afya ya mwaka 2007, huduma za
tiba hutolewa bure kwa makundi maalum, au kwa kuchangiwa kwa sehemu ya
gharama, au kwa kupitia mfumo wa Bima mbalimbali za Afya kama vile CHF.
Kwa wale wasio na uwezo na wanaothibitishwa kuwa hawana uwezo, utaratibu
wa msamaha hutumika.
Katika
kuhakikisha kwamba wananchi wanaohitaji dawa ya sumu ya nyoka
wanahudumiwa ipasavyo, Mhe. Ummy Mwalimu, Waziri wa Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto anatoa maelekezo yafuatayo:-
Waganga Wakuu
wa Mikoa na Viongozi wa Hospitali zote nchini wahakikishe kuwa Hospitali
zote za umma zinaingiza dawa hii katika dawa za dharura ili iweze
kununuliwa kama dawa zingine za dharura kupitia kifungu cha fedha za
dawa za dharura.
Kwa wagonjwa
ambao watakuwa na Bima ya Afya, basi gharama za matibabu hayo zitalipwa
kwa kupitia utaratibu huo wa Bima. Wananchi wanahimizwa kujiunga na Bima
za Afya (CHF/NHIF) ili kupata unafuu wa matibabu haya na mengine. Mfano
CHF - gharama ya kujiunga katika Halmashauri mbalimbali kwa kaya ni
kati ya shilingi 5,000/= hadi shilingi 30,000/= kwa mwaka.
Kwa wagonjwa
ambao watakuwa hawana Bima ya Afya, hao watatakiwa kuchangia gharama
hiyo kwa nusu ya bei ya gharama ya dawa hizi au kwa kiwango kingine
kitakachoamuliwa na Mganga Mkuu wa Serikali kadri itavyohitajika. Hii ni
kutokana na ukweli kwamba kung'atwa na nyoka ni ajali na wananchi wengi
wanaopatwa na ajali hii wapo maeneo ya vijijini ambao kimsingi uwezo
wao wa kumudu gharama hizi kubwa za matibabu ya dawa ya sumu ya nyoka ni
mdogo.
Wagonjwa
watakaothibitika kuwa hawana fedha za kuchangia gharama hiyo, basi
hospitali husika kwa kupitia mpango wa msamaha wa kulipia huduma za afya
wahakikishe kwamba wanampatia mgonjwa huduma hizo kwa utaratibu wa
msamaha wa gharama hizo.
Aidha, kwa kuwa
nchi yetu ni kubwa na ina nyoka wengi, Mhe Waziri wa Afya anawaagiza
Waganga Wakuu wa Mikoa na Halmashauri zote nchini kupitia kwa uangalifu
takwimu za wagonjwa walioumwa na nyoka katika kipindi cha kuanzia mwaka
2013 hadi 2016 na kuziwasilisha Wizarani kabla ya tarehe 31 Januari
2017 ili kupata takwimu za mahitaji halisi ya dawa ya sumu ya nyoka
nchini. Hii itasaidia kuboresha upangaji, uagizaji na upatikanaji wa
dawa hizo nchini.
Vile vile,
Waziri wa Afya ameiagiza Bohari ya Dawa (MSD) kuweka utaratibu wa
haraka wa kununua dawa hizo moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji ili
kupata unafuu wa bei.
0 comments:
Post a Comment