Nchini kenya waziri wa fedha Henry 
Rotich leo amewasilisha bungeni bajeti ya makadirio ya matumizi ya pesa 
za serikali katika kipindi cha mwaka 2016-2017.
Bajeti hiyo ya 
jumla ya shilingi trilioni 2.26 inatarajiwa kufadhiliwa kupitia 
ukusanyaji wa ushuru na mikopo kutoka kwa washirika wa kimaendeleo. 
Serikali inalenga kukopa shilingi bilioni 778 hatua ambayo itaongeza 
deni la kenya ambalo kufikia sasa ni shilingi trilioni 3.32.
Matumizi
 zaidi itaelekezwa kwa ujenzi wa miundo mbinu ikiwa ni pamoja ujenzi wa 
reli ya kisasa, kuimarisha usalama, huduma za afya na pia kuziwezesha 
serikali za majimbo.
Kama ilivyo ada bajeti inaposomwa kuna wale 
wa wanaofaidi na wale wanaopoteza. Gesi ya kupikia na chakula cha mifugo
 umeondolewa ushuru, Huku ushuru wa petroli na mafuta taa ukiongezwa. 
Bidhaa za mafuta ya urembo zikiwekewa ushuru wa asilimia kumi kwa mara 
ya kwanza.
Waziri ametenga shilingi bilioni 4.3 kwa huduma za bure
 za wanawake wajawazito kujifungua,milioni 19.7 kwa maandalizi ya 
uchaguzi mkuu wa mwaka 2017 na shilingi milioni 7.9 kwa watoto mayatima.
 
Nchini Tanzania makadirio ya bajeti ya mwaka 2016 na 2017 ni trilioni
 29,5 pesa za Tanzania ikiizidi bajeti ya mwaka wa 2015 na 2016 kwa 
trilioni 7.1.
Waziri wa Fedha nchini Tanzania Phillip Mpango 
alisema kuwa kati ya fedha hizo, Shilingi trilioni 18.46 zitatokana na 
jumla ya mapato ya ndani.
Kiwango hicho kimezidi shilingi trilioni 3.64 za bajeti iliyopita ambayo ililenga kukusanya shilingi trilioni 4.82.
Shilingi
 trilioni 17.72 zitakuwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida, huku trilioni
 11.82 sawa na asilimia 40 ya bajeti nzima, zikitengwa kwa ajili ya 
shughuli za maendeleo.
Bwana Mpango alisema washirika wa maendeleo
 wanatarajiwa kuchangia shilingi trilioni 3.6, ikiwa ni ongezeko la 
shilingi trilioni 1.7 ikilinganishwa na shilingi trilioni 1.88 
zilizokuwa zinategemewa kwenye bajeti iliyopita.

Makadirio ya bajeti nchini Uganda mwaka 2016 na 2017 iliyosomwa leo 
ni ya jumla ya dola bilion 7.5 ambayo ni sawa na trillioni 27. 3 pesa za
 Uganda, tofauti na bajeti ya mwaka uliopita ya mwaka 2015 na 2016 
ambayo ilikuwa ni dola bilioni 6.9.
Bajei kubwa mwaka huu nchini 
Uganda imeelekezwa kwa wizara ya kazi na uchukuzi ambayo ilipewa dola 
blioni 1.1 huku wizara ya ulinzia ikipewa dola milioni 435. Wizara ya 
afya imepata dola milioni 525.
Wizara ya nishati na maendeleo ya 
madini ilipata dola milioni 695 huku Wizara ya kilimo ambayo nidiyo 
muhimu nchi Uganda ikiewa dola milioni 522.