Mkazi wa Dar es Salaam, Goodluck Madaraka anayedaiwa kujeruhiwa na 
risasi wakati wa mkesha wa sherehe ya harusi eneo la Tabata Kisukulu 
usiku wa kuamkia jana, akiwa katika eneo hilo lililogeuka kuwa la msiba 
jana, baada ya mwenzake Salim Ally kudaiwa kuuawa kwa risasi na jirani 
yao aliyekerwa na kelele za muziki wakati wa sherehe hiyo. Picha na 
Kalunde Jamal  
Katika hali isiyokuwa ya kawaida, mwanamume mmoja amewafyatulia
 risasi watu wawili na kusababisha kifo cha mmoja kwa kile kinachodaiwa 
kumletea usumbufu wakati wa mkesha wa harusi. 
Mkuu wa Upelelezi  wa Mkoa wa Ilala, David 
Mnyambuga amethibitisha kutokea kwa tukio hilo ingawa hakuwa tayari 
kulizungumzia kwa madai kuwa siyo msemaji na anayetakiwa kufanya hivyo  
ni Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala ambaye hakupatikana kulizungumzia 
hilo.
Majeruhi wa tukio hilo, Goodluck Madaraka 
aliyejeruhiwa na risasi zilipokuwa zinapigwa hewani, alisema saa tano na
 nusu usiku walipokuwa wanacheza muziki kwenye mkesha wa harusi, ghafla 
jirani yao aliyefahamika kwa jina la Lucas Muhabe alikuja na panga na 
kuwafukuza kwa madai kuwa wanampigia kelele.
Alisema Muhabe aliondoka na baada ya muda alirudi 
na bastola na kupiga risasi ovyo na kwa bahati mbaya ikampata begani 
Mahamudu Muhasi aliyekuwa anapita njia na kumpiga nyingine ya kichwa na 
kumuua papo hapo.
“Muhasi alikuwa anapita njia hivyo hata vijana 
walivyokimbia yeye hakukimbia na alipopigwa risasi ya bega la kushoto 
alilalama kumwambia huyo baba kuwa anamwonea kwani hafahamu kitu 
chochote, cha kushangaza baada ya kuambiwa hivyo aligeuka na kumpiga 
nyingine ya kichwa na kufariki dunia papo hapo,” alisema Madaraka.
Madaraka alisema kuwa kwenye heka heka za kupigwa 
risasi hizo moja ilimpitia kwenye shavu na kumpasua na alikwenda 
Hospitali ya Amana na kushonwa nyuzi tatu.
Kaka wa marehemu, Salim Ally alisema kuwa Muhasi 
alikuwa anashinda kwake na kulala kwa mjomba wake mbali kidogo kutoka 
kwake, siku ya tukio baada ya kula chakula cha usiku na kuzungumza hadi 
saa tano usiku, alimsindikiza.
Alisema alipohakikisha wamepita kwenye maeneo 
ambayo hakuamini kama ni salama, alimwacha aende mwenyewe, njia kuu 
ikiwa ni hapo palipokuwa na mkesha wa harusi na alipata taarifa ndugu 
yake ameuawa kwa kupigwa risasi.
“Amekuja mwezi wa saba kutoka Malinyi Ulanga, siyo
 mwenyeji na wala hashindi maeneo hayo, ndiyo maana hata wakati vijana 
wanakimbia alikuwa anashangaa tu ndiyo akapigwa risasi, inauma sana hata
 siamini kama sheria itachukua mkondo wake kwa jinsi ninavyoumia,” 
alisema Ally.
Ally aliongeza kuwa, tunasikia mtuhumiwa amesema 
marehemu ni jambazi ndiyo maana amempiga risasi, kitu ambacho siyo kweli
 hana historia hiyo na ni mgeni hapa jijini.
Akizungumza na gazeti hili Mtawala Amani ambaye 
nyumbani kwake ndiyo kulikuwa na mkesha wa harusi, alisema muda wa saa 
tatu aliamua kujipumzisha barazani aliamshwa mnamo saa tano na nusu na 
kelele zilizokuwa zinatokea nje ya nyumba yake.
Alisema baada ya kutoka nje alikuta damu na mwili 
wa kijana Muhasi na kuambiwa kuwa jirani yao Lucas Muhabi ndiyo amemuua 
kwa kumpiga risasi na muda siyo mrefu polisi walifika na kuuchukua mwili
 kuupeleka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Mke wa Amani, Pili Miraji alisema kuwa anamfahamu marehemu kwa kuwa alikuwa akimwona anapita maeneo hayo na anakwenda kwa mjomba wake ambako siyo mbali kutoka hapo kwao.
Mke wa Amani, Pili Miraji alisema kuwa anamfahamu marehemu kwa kuwa alikuwa akimwona anapita maeneo hayo na anakwenda kwa mjomba wake ambako siyo mbali kutoka hapo kwao.
 RSS Feed
 Twitter

9:24 AM
MZM

0 comments:
Post a Comment