Wednesday, April 29, 2015


Maelfu ya maafisa wa polisi nchini Marekani wameamriwa kuwasaidia maafisa waliozingirwa mjini Baltimore, baada ya ghasia zilizosababishwa na waandamanaji waliojawa na hasira, kufuatia kifo cha Mmarekani mweusi.
Muandamanaji akiwafokea polisi waliokuwa wanajaribu kudhibiti hali mjini Baltimore
Watu 27 wametiwa nguvuni huku polisi 15 wakijeruhiwa wakati waandamanaji hao wengi wao wanafunzi waliokuwa wanarusha mawe na kupora biashara za watu, walipopambana na maafisa wa polisi.
Ghasia mjini Baltimore zilianza baada ya mazishi ya kijana Mmarekani mweusi kwa jina Freddie Gray, aliyekuwa na miaka 25 na aliyefariki tarehe 19 mwezi wa Aprili kufuatia majeraha mabaya ya uti wa mgongo aliyoyapata wakati alipokuwa anatiwa nguvuni na maafisa wa polisi.

Mmoja wa waandamanaji akiharibu gari la polisi mjini Baltimore
Licha ya maombi ya kudumisha amani kutoka kwa familia ya kijana huyo, vijana mjini Baltimore walimiminika mitaani na kuzua vurugu, kuchoma magari, kupora maduka na kuharibu biashara za watu.
Kufuatia visa hivi Meya wa Baltimore Stephanie Rawlings-Blake ametangaza amri ya kutotoka nje kuanzia usiku wa leo na kuamuru shule za mji huo kufungwa kwa siku moja.
Stephanie Rawlings amesema hawatakubali wezi na wahalifu kuuharibu mji wa Baltimore kwa vurugu na ghasia.
"Watu wengi wametumia muda mwingi kujenga mji huu, hatuwezi kuwaacha wahalifu kuuharibu mji ambao watu wengi wameupigania," alisema meya Rawlings Blake.
Maafisa sita wasimamishwa kazi kwa Muda kupisha uchunguzi
Hizi ni vurugu za hivi karibuni kabisa katika mfululizo wa makabiliano kati ya polisi wa Marekani na vijana Wamarekani weusi waliojawa na hasira kwa kile wanachokiita ubaguzi unaofanywa dhidi yao na maafisa wa polisi.
Huku hayo yakiarifiwa maafisa wapatao sita wamesimamishwa kazi kwa muda kupisha uchunguzi unaofanwa juu ya mauaji ya Freddie Gray, ambapo ripoti ya uchunguzi huo inatarajiwa kukabidhiwa waendesha mashtaka wa jimbo la Maryland.
Polisi wa mjini Baltimore katika jimbo la Maryland
Lakini idara ya sheria nchini Marekani ambayo tayari ilikuwa imeshaanza uchunguzi juu ya utumiaji wa nguvu kupita kiasi unaodaiwa kufanywa na polisi wa Baltimore imefungua uchunguzi juu ya haki za binaadamu
Hata hivyo polisi imekiri kwamba Kijana Freddy Gray aliomba kupewa matibabu kwa kupewa kifaa cha kuvutia pumzi baada ya kuzuiliwa na kukiri kwamba gray angepaswa kupewa matibabu mapema.
Kisa hiki kinatokea miezi kadhaa baada ya kisa cha kupigwa risasi mmarekani mweusi ambaye hakuwa na silaha Michael Brown na afisa mmoja wa polisi mjini Ferguson, Missouri hali iliosababisha maandamano makubwa.

0 comments: