Tuesday, April 21, 2015






Serikali imerejesha mafunzo ya madereva kila baada ya miaka mitatu wakati wa kumalizika kwa muda wa leseni zao, huku ikifafanua kuwa elimu watakayoipata ina umuhimu katika kazi zao, kutokana na mabadiliko mbalimbali yanayotokea katika sekta hiyo.

 

Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Makongoro Mahanga, alitangaza uamuzi huo wa Serikali jana katika mkutano kati yake na viongozi wa madereva wa mabasi nchini.

 

Mkutano huo umefanyika kama ilivyoahidiwa na Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka, wakati alipokuwa akijitahidi kumaliza mgomo wa madereva uliofanyika Aprili 10 mwaka huu, wakati walipokuwa wakipinga pamoja na mambo mengine, sharti la kwenda shule ili kupata leseni mpya.

 

Madereva hao walitaka Serikali ifanyie marekebisho Sheria ya Usalama Barabarani, kwa kuondoa kipengele kinachowataka madereva kwenda Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kwa mafunzo ya muda mfupi kila wakati leseni zao zinapoisha, ili kupata sifa ya kupata leseni nyingine.

 

Sababu ya kupinga kupata mafunzo, ilidaiwa kuwa utaratibu huo uliotangazwa Machi 30, mwaka huu, ulianzishwa bila kushirikisha madereva katika kuuandaa.

 

Pia walipinga kutakiwa kujilipia gharama za shule hiyo ambazo walidai ni Sh 560,000 kwa magari ya kawaida na Sh 200,000 kwa magari ya abiria.

 

Sababu nyingine iliyochangia wapinge shule hiyo, walidai ni kukosekana kwa mikataba ya ajira, inayoweza kuwahakikishia kulindwa kwa kazi zao hadi wanapomaliza mafunzo.

 

Madai mengine yaliyokuwa nje ya shule hiyo, madereva hao walitaka kuondolewa kwa faini ya Sh 300,000 kwa kila kosa la barabarani na kuitaka Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchikavu (Sumatra), kuhakiki uhalisia wa dereva anayeandikishwa na mmiliki wa chombo husika.

 

Majibu ya Serikali Mahanga aliyekuwa Mwenyekiti wa kikao hicho, alisoma tamko la Serikali lililoeleza kuwa pamoja na kurejesha mafunzo hayo, utekelezaji wake hautafanyika mara moja kwa kuwa Kanuni zake hazijakamilika.

 

“Tangazo hili (la kwenda shule) limetolewa kwa kuzingatia umuhimu wa mafunzo kazini kwa wafanyakazi na madereva kama ilivyo kwa wafanyakazi wengine,” alisema Mahanga.

 

Alisisitiza kuwa baada ya miaka mitatu ya leseni, dereva atatakiwa kupata mafunzo mafupi, ambayo ni kati ya siku tatu hadi saba na atakayegharimia mafunzo hayo ni mwajiri, si mfanyakazi na ni katika chuo chochote kinachotambulika.

 

Akifafanua, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani, Mwamini Malemi aliyekuwepo katika mkutano huo, alisema mitaala ya mafunzo hayo bado inaandaliwa, hivyo si rahisi Kanuni hiyo kuanza kutekelezwa mwaka huu hata kama zitakamilika.

 

Kuhusu mikataba ya ajira ambayo ililalamikiwa mno na madereva wakati wa mgomo, Mahanga alisema Serikali itapitia upya mikataba hiyo ili kuhakikisha mambo yote muhimu yanazingatiwa.

 

Akiongezea hoja katika suala la mikataba, Malemi alisema ni lazima mikataba iwe imekamilika kabla ya kuanza kutumika kwa kanuni ya kwenda shule, ili ioneshe wajibu wa mwajiri katika kumsomesha mfanyakazi.

 

Kuhusu kauli iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova ya kuondoa tochi za kupima mwendo kasi barabarani, Mahanga alisema matumizi ya tochi zinazotumika kupima mwendo kasi na ratiba ni sehemu ya utekelezaji wa Sheria za Usalama Barabarani.

 

Hoja nyingine Katika kikao hicho mbali na hoja zilizosababisha mgomo, kulikuwa na hoja nyingine zilizowasilishwa, ikiwemo changamoto ya madereva kupata maelekezo yanayokinzana kutoka Jeshi la Polisi na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchikavu na Majini (Sumatra), kuhusu ratiba ya kuondoka wanakotoka na kuwasili wanakokwenda.

 

Akitoa majibu ya Serikali, Mahanga alisema amepokea hoja hiyo na ataifanya utafiti wa kina. Katika hoja ya kuwataka waajiri kuongeza posho za kazi, Mahanga alisema Serikali haiwezi kupanga posho za madereva katika kikao hicho, kwasababu kila mwajiri ana uwezo wake kulingana na safari za gari yake.

 

Hata hivyo, aliahidi kufanyika utafiti suala hilo katika nchi nyingine, ili aone namna ambavyo madereva wengine wamekuwa wakilipwa posho.

 

Serikali pia imeahidi kuimarisha ukaguzi sehemu za kazi kwa kushirikiana na Sumatra, utakaohusu wamiliki wa magari na kuhuisha mfumo wa kumbukumbu, utakaoonesha kila gari na dereva wake halisi na kuweka vitambulisho vya dereva katika kila gari analoendesha.

 

Mahanga alisema Serikali pia itaweka utaratibu mpya ambapo dereva mwenyewe atajiwekea bima ya ajali itakayoanzishwa na kujiunga na vyama vya wafanyakazi, ili watetee mikataba yao ili iweke pia maswala ya bima hizo.

 

Alisema pia Serikali imeanzisha Mfuko wa Fidia ya Wafanyakazi, ambao utaanza hivi karibuni, ambao mwajiri atawajibika kuchangia.

 

Chama cha Wafanyakazi  Kuhusu chama cha wafanyakazi, Mahanga alisema Serikali imepokea pendekezo la kusaidia madereva kuunda chama cha wafanyakazi chenye nguvu, ambapo alisema kumbukumbu zinaonesha madereva wana vyama vilivyosajiliwa kwa Msajili wa Vyama vya Wafanyakazi na Waajiri.

 

Alitaja vyama hivyo kuwa ni Umoja wa Wafanyakazi wa Mawasiliano na Usafiri Tanzania (COTWU), kilichosajiliwa mwaka 2000 na Chama cha Wafanyakazi cha Usafiri wa Barabara (TARWORTU) kilichosajiliwa mwaka 2013.

 

“Katika kushughulikia changamoto za wafanyakazi na mwajiri wote mnategemeana, jambo mtakalofanya ni kuanzisha majadiliano kupitia vyama vya wafanyakazi lakini kwanza muwe ndani ya vyama,” alisema Mahanga.

 

Wanung’unika  Baada ya kusomwa kwa tamko hilo la Serikali, Katibu Mkuu wa Vyama vya Madereva Tanzania, Mwanarashidi Salehe, alisema mafunzo wanayotakiwa kuchukua hayana tija yoyote, kwa kuwa wakufunzi ni wa kizamani na pia magari yanayotumika ni ya kizamani, ambayo hayaongezi chochote katika kazi yao.

 

“Kwanza hakuna kipya katika mafunzo hayo, mimi nimehudhuria mara mbili....pili katika kikao hiki tulitarajia tutakutana na wamiliki wa magari ambao ndio waajiri wetu ili waseme waliyonayo juu yetu na sisi tuseme yetu tujadiliane na kupata majibu,” alisema Salehe.

 

Mwenyekiti wa chama hicho, Clement Masanja alisema mikataba waliyonayo madereva ni dhaifu mno, haioneshi mambo ambayo dereva atanufaika nayo.

 

“Tulitarajia katika kikao hiki tutatoka na majibu ya posho za madereva, ili dereva ajue atalipwa kiasi gani kwa safari za ndani na nje ya nchi kwa sababu anavyolipwa ni manyanyaso matupu,” alisema Masanja.

0 comments: