Saturday, December 12, 2015

Burundi
Watu zaidi ya 200 wameuawa Burundi tangu kuanza kwa machafuko Aprili
Miili zaidi ya 34 imepatikana katika barabara za mji mkuu wa Burundi huku machafuko yakiendelea.
Mwandishi wa BBC ameona maiti 21 katika mtaa mmoja wa Bujumbura na maafisa wa serikali wamesema kuna miili mingine 13.
Maiti nyingi zinaonekana kuwa za vijana waliouawa kwa kupigwa risasi, baadhi wakiwa wamefungwa mikono yao ikiwa pamoja mgongoni.
Miili hiyo imepatikana siku moja baada ya watu wenye silaha kushambulia maeneo matatu ya jeshi.
Machafuko yameendelea kutatiza Burundi tangu kutibuliwa kwa jaribio la kupindua serikali mwezi Mei na maandamano yaliyofanyika kupinga hatua ya Rais Pierre Nkurunziza kuwania urais kwa mara nyingine, wazo alilotangaza Aprili.
Bw Nkurunziza alishinda uchaguzi uliofanyika Julai.
Idadi kubwa ya miili imepatikana mtaa wa Nyakabiga, Burundi ambao umeshuhudia maandamano ya kupinga serikali.
Mingine ilipatikana mtaa wa kusini wa Musaga. Kuna ripoti za kupatikana kwa miili katika maeneo mengine ya mji huo.
Wakazi wanawatuhumu maafisa wa pilisi kwa kuwakamata vijana wakati wa misako ya nyumba kwa nyumba Ijumaa na kisha kuwaua.
Lakini msemaji wa polisi ameambia Reuters kwamba waliouawa walihusika katika kushambulia maeneo ya serikali.

0 comments: