Kumekucha. Pengine hilo ndilo neno linalofaa kutumika kuelezea matokeo ya utafiti kuhusu
Dar es Salaam. Kumekucha. Pengine hilo ndilo neno linalofaa
kutumika kuelezea matokeo ya utafiti kuhusu kinyang’anyiro cha urais
katika Uchaguzi Mkuu 2015 ambayo yanaonyesha kuwa iwapo ungefanyika leo,
Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa angeibuka mshindi.
Wakati
Lowassa angeibuka na ushindi kwa asilimia 13 na Waziri Mkuu, Mizengo
Pinda angefuatia kwa karibu akiwa na asilimia 12 huku Katibu Mkuu wa
Chadema, Dk Willibrod Slaa akiwa wa tatu kwa asilimia kumi na moja.
Hata hivyo, asilimia 33 ya wananchi waliohojiwa walisema bado hawajaamua wampigie kura mgombea gani.
Utafiti
huo wa Taasisi ya Twaweza unayoonyesha wagombea hao kukabana kwa
tofauti ya asilimia mojamoja na ambao ulitangazwa Dar es Salaam jana,
ulifanywa Septemba 2014 kwa kuwahoji wananchi 1,445 kutoka Tanzania
Bara.
Akitangaza matokeo hayo, mtafiti wa Twaweza,
Elvis Mushi alisema utafiti huo ni wa tatu kufanyika nchini na kwamba
awamu ya kwanza ilifanyika mwaka 2012 na Lowassa alipata asilimia sita
kabla ya mwaka jana na mwaka huu kuibuka na asilimia 13.
Akimzungumzia
Pinda, mtafiti huyo alisema mwaka 2012 alipata 16, lakini zilishuka
mwaka 2013 hadi kufikia asilimia kumi na moja na kupanda tena mwaka huu
hadi 12.
“Kwa upande wa Dk Slaa, mwaka 2012 na 2013 alipata asilimia 19 lakini sasa ameshuka hadi asilimia kumi na moja,” alisema Mushi.
Wagombea
wengine waliotajwa na asilimia zao kwenye mabano ni Profesa Ibrahim
Lipumba (6%), Dk John Magufuli (3%), Freeman Mbowe (3%), Samuel Sitta
(4%), Bernard Membe (5%) na Zitto Kabwe (1%).
“Hata
hivyo, kitu muhimu cha kuangalia katika ripoti hii siyo tu majina ya
mgombea, bali ni idadi ya wananchi asilimia 33 ambao wamesema hawajui
watamchagua nani,” aliongeza Mushi.
Ripoti hiyo
inaonyesha kuwa iwapo vyama vyote vya upinzani vitaungana na kumchagua
mgombea urais mmoja, asilimia 41 ya wananchi waliohojiwa walisema
wangemchagua Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa, akifuatiwa na
Profesa Lipumba (14%), Mbowe (11%) na Zitto Kabwe (6%).
Wanasiasa
wengine waliotajwa ni Tundu Lissu, Maalim Seif Sharif Hamad, James
Mbatia na Augustino Mrema ambao kila mmoja aliambulia asilimia moja.
Wengi kuchagua CCM
Pia
utafiti unaeleza kuwa iwapo Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa)
utasimamisha mgombea mmoja wa urais dhidi ya CCM, asilimia 47 ya
wananchi walisema wangeichagua CCM huku asilimia 28 wangempigia kura
mgombea wa muungano wa upinzani. Asilimia 19 ya wananchi walisema
watampigia kura mgombea bila kujali chama chake.
“Kura
za kundi hili zitategemea ubora wa wagombea. Kama kura hizo zitagawanywa
kwa CCM na upinzani, CCM itashinda urais kwa kuzidi upinzani kwa kura
nyingi kiasi. Kutakuwa na kitisho kwa ushindi wa CCM endapo wapigakura
wote watamchagua mtu badala ya chama watampigia mgombea wa upinzani,
kitu ambacho kina uwezekano mdogo kutokea,” inasema ripoti hiyo.
Wananchi walia uchumi, afya na elimu
Wananchi
walipoulizwa ni matatizo gani matatu makubwa yanayoikabili Tanzania
walitaja ukosefu wa elimu bora, afya na hali mbaya ya kiuchumi na kwamba
matatizo hayo yameshika nafasi ya juu kwa miaka mitatu mfululizo.
“Umaskini
umeongezeka kutoka asilimia 49 mwaka 2012 hadi 63 mwaka 2014, huku
matatizo ya afya yakiongezeka kutoka asilimia 40 hadi 47 na elimu
imeshuka kutoka asilimia 46 mwaka jana hadi 38 mwaka huu,” alisema
Mushi.
Wabunge na ahadi zao
Katika
utafiti huo, imeelezwa kuwa ahadi nyingi zilizotolewa na wabunge kwenye
mikutano ya kampeni wakati wa uchaguzi hazijatekelezwa na kwamba
asilimia 78 ya wananchi bado wanazikumbuka.
Ahadi
nyingi zilizotolewa na wagombea zilihusu miradi ya ujenzi barabara,
maji, ujenzi wa hospitali, kuboresha elimu, umeme, mikopo kwa vikundi,
kuongeza ajira, kujenga madaraja na kuboresha kilimo.
Pia
ripoti imeweka wazi kuwa karibu nusu ya wabunge wote huenda wasirudi
tena katika nyadhifa zao. Asilimia 47 ya wananchi walioulizwa iwapo
watampigia tena kura mbunge wao walisema hapana huku asilimia kama hiyo
wakisema ndiyo.
Akizungumzia utafiti huo, mwandishi wa
habari mkongwe nchini, Jenerali Ulimwengu alihoji namna majina ya
wagombea yaliyotajwa kwenye ripoti hiyo yalivyopatikana huku
akipendekeza namna sahihi ya kuwalinganisha wagombea hao.
“Walitakiwa
kulinganishwa kwa mfano kwenye kilimo, watuambe Mizengo Pinda anaweza
kufanya nini akilinganishwa na mgombea mwingine. Vinginevyo inakuwa ni
mashindano ya urembo. Tunatumia muda mrefu kumchagua mbuzi Vingunguti
kumbe atachinjwa kesho,” alisema Ulimwengu.
Kwa upande
wake, Dk Benson Bana wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alisema
hatashangaa kusikia kuna watu wengine wametoa ripoti nyingine kupinga
utafiti huo kwa kuwa kumekuwapo na utamaduni wa kutokukubaliana na
matokeo ya namna hiyo.
“Tafiti hupingwa na tafiti, kwa
hiyo mtu asianze kupinga tu, fanya kama wao (Twaweza) jifunze kutumia
takwimu,” alisema huku akionyesha kukasirishwa na watu waliokuwa wakitoa
maoni ya kupinga ripoti hiyo.
Kauli ya Nape
Katibu
wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema anakubaliana na
matokeo hayo kwa kuwa yamepatikana na njia ya simu katika nchi ambayo
ina watumiaji wengi wa aina hiyo ya mawasiliano.
Hata
hivyo, alisema: “Tatizo ahadi nyingi zinazotolewa na viongozi kwa
wananchi hazitekelezwi. Tunasema asilimia 80 ya Watanzania ni wakulima
lakini asilimia mbili ya viongozi ndiyo walioahidi kuhusu kilimo.”
Mjumbe
wa lililokuwa Bunge la Katiba, Maria Sarungi alisema ripoti hiyo haina
habari njema kwa vyama vya siasa kwa sababu inaonyesha kuwa wananchi
wamekosa imani ya kupata msaada, badala yake wameanza kumtafuta
‘mkombozi’ atakayewasaidia.
“Inapotokea asimilia 41
wanasema hawajui watamchagua nani huku asilimia 10 wakisema inategemea
na mtu atakayejitokeza inaonyesha wananchi wanamtafuta mtu
atakayewasaidia na siyo chama.
“Mambo ya wananchi yanatatuliwa na Katiba, tatizo la utawala bora na umaskini haliletwi na vyama vya siasa linaletwa na Katiba.”
0 comments:
Post a Comment