Thursday, July 16, 2015

WAKILI Felix Kiprono aliyegonga vichwa vya habari baada ya kutoa azma yake ya kumuoa bintiye Rais Barack Obama, Malia sasa ametangaza kuwa ameamua kujiunga na dini ya Kiislamu.
Kiprono, 24 aliambia Taifa Leo katika mahojiano kuwa atalichukua jina la Kiislamu la Adnan punde tu atakapomaliza masomo yake ya dini yaitwayo Tawhid.
“Natarajia kuyamaliza masomo yangu ya Tawhid niliyoyaanza mwaka wa 2012 nilipopewa cheti cha kubadili dini,” alisema Kiprono.
Wakili huyo amesema alipokea cheti chake mwaka wa 2012 baada ya kuongozwa na binti mmoja wa Kiislamu aliyemuenzi kwa upole wake na maadili yake.
“Binti huyo alinifunza mengi kuihusu dini hiyo na nilipokata kauli kusilimu akanijulisha kwa masheikh na nikapata cheti katika Msikiti wa Jamia jijini Nairobi,” aliongeza.
Kiprono alisema atakamilisha mafunzo ya dini mwezi Oktoba na baadaye kuyabadilisha majina kwenye stakabadhi zake ili kuliongeza jina la Kiislamu, Adnan.
Aliongeza kuwa amekuwa akiyafuata maadili na mafunzo ya dini hiyo na hata kufunga katika mwezi mtukufu wa Ramadhan.
“Nimepata amani tele kwa kujiunga na dini hii na hivyo sitarajii kubatili uamuzi wangu kamwe,” alisema Kiprono.
Wakili huyo aligonga vichwa vya habari miezi za mwanzo wa 2015 alipotangaza kuwa angetaka kumuoa bintiye Rais Obama na kulipa mahari ya ng’ombe 50, kondoo 70 na mbuzi 30, kiwango alichosema kimewekwa na utamaduni wa kabila analotoka.

Kusubiri mwaliko rasmi
Aidha, wakili huyo amebatili uamuzi wake wa kukutana na Rais Obama atakapofika nchini Kenya wiki ijayo kwani amesema kuwa atasubiri kualikwa na mashemeji wake watarajiwa.
“Katika mila zetu kama waafrika mwanamume hana uhuru wa kukutana na mashemeji wake bila mpangilio maalum kutoka kwa wazee wa kijiji hivyo sitamtafuta Rais Obama atakapokuwa nchini kwani nina Imani ombi langu alilipata na atalishughulikia,” alisema Kiprono.
Kiprono aliongeza kuwa hatomtafuta pia bintiye Rais kwani ni msichana mdogo ambaye hajatimiza umri wa kufanya uamuzi wa ndoa.
“Angali msichana mdogo na hivyo kufanya urafiki wa kimapenzi naye itakuwa ni kukiuka sharia hivyo nitasubiri uamuzi wa wazazi wake,” alisema Kiprono.
Wakili huyo anaendelea na masomo ya uzamili wa sheria katika chuo kikuu cha Oxford Uingereza.

0 comments: