Benki ya Afrika ya Maendeleo, ADB imepata rais mpya, waziri wa kilimo wa
Nigeria Akinwumi Adesina, ambaye amewashinda wapinzani 7 katika duru 6
za uchaguzi. Anachukua nafasi ya Donald Kaberuka anayemaliza muda wake.
Akinwumi Adesina aliibuka mshindi baada ya duru sita za uchaguzi,
zilizomalizika jana jioni katika makao makuu ya Benki ya Afrika ya
Maendeleo mjini Abidjan, Cote d'Ivoire. Adesina, msomi mwenye shahada ya
uzamili katika masuala ya uchumi na maendeleo, anachukua hatamu za
benki hiyo ambayo inajikuta katika mazingira mapya kifedha barani
Afrika.Baada ya kupata ushindi wa karibu asilimia 60 ya wajumbe wa bodi ya magavana wa benki hiyo, Akinwumi Adesina alisema atakuwa rais mwenye kujituma.