Saudi Arabia imesema majeshi yake yamewauwa na waasi wa Yemen waliofanya
shambulizi lao la kwanza kubwa dhidi ya nchi hiyo tangu kuanza mwezi
uliopita mashambulizi ya angani yanayoongozwa na Saudia
Wizara ya ulinzi ya Saudi Arabia imesema wanajeshi wake watatu pia
waliuawa katika mapambano hayo baada ya waasi wa Houthi kuvilenga vituo
vyao vya uangalizi, wakati jeshi lake likijaribu kuzuia shambulizi hilo.
Kumekuwa na makabiliano hapo kabla lakini hii ni mara ya kwanza ambapo
jeshi la Saudi Arabia limeripoti kuhusu shambulizi kamili la waasi wa
Houthi katika mipaka yake. Katika mji mkuu Sanaa, mashambulizi mapya ya
kutokea angani yanayoongozwa na Saudia yamefanywa katika uwanja wa ndege
ikiwa ni siku chache tu baada ya ndege za kivita kuilipua njia ya ndege
katika uwanja huo ili kuzuia ndege moja ya Iran kutua.
Wakati huo huo, mawaziri wa mataifa ya Ghuba hapo jana walipinga
pendekezo la kuandaa mazungumzo katika nchi isiyounga mkono upande
wowote katika mzozo wa kisiasa nchini Yemen, wakati ripoti ya watalaamu
ikisema kuwa Iran imekuwa ikiwapa silaha waasi wa Houthi tangu mwaka wa
2009.
Umoja wa Mataifa unajaribu kumaliza operesheni ya angani iliyodumu wiki
kadhaa, na kuzirejesha pande zote mbili katika meza ya mazungumzo. Baada
ya mkutano wa mjini Riyadh, mawaziri wa nchi za Ghuba walisisitiza kuwa
mazungumzo baina ya makundi hasimu ya kisiasa nchini Yemen yaandaliwe
nchini Saudi Arabia, ambayo inaongoza muungano wan chi za Kiarabu dhidi
ya waasi wa Kishia tangu Machi.
Iran inapendekeza kuandaa mazungumzo ya Umoja wa Mataifa ili kumaliza
vita nchini Yemen katika taifa lisiloegemea upande wowote, ambalo
haliwakilishwi katika muungano unaoongozwa na Saudia.
Baraza la Ushirikiano wa Ghuba lenye nchi sita wanachama limesisitiza
kuunga mkono juhudi kali zinazofanywa na serikali halali ya Yemen za
kuandaa mkutano chini ya mwamvuli wa Baraza hilo mjini Riyadh.
Katibu Mkuu wa Baraza hilo Abdullatif al-Zyani amesema mkutano huo
utahudhuriwa na “pande zote za Yemen na zinazounga mkono uhalali na
usalama na uimara wa Yemen”.
Mkutano wa jana wa nchi za Ghuba ambazo ni Bahrain, Kuwait, Oman, Qatar
na Umoja wa Falme za Kiarabu, ulilenga kuweka msingi wa mkutano mkuu wa
viongozi wa Baraza hilo utakaoandaliwa Jumanne wiki ijayo, na ambao pia
utahudhuriwa na Rais wa Ufaransa Francois Hollande.
Mgogoro huo umeongeza mivutano katika kanda hilo. Iran inayotuhumiwa kwa
kuwapa silaha waasi wa Houthi, imesema meli zake mbili zilizotumwa
katika Ghuba ya Aden zimefika mlango wa Bab al-Mandab, njia muhimu ya
bahari baina ya Yemen na Djibouti. Iran inasisitiza kuwa meli zake hizo
hazitafika katika mipaka ya bahari ya nchi nyingine.
0 comments:
Post a Comment