KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida, wanafunzi wa shule za msingi za Mwangaza na Ngarenaro, juzi walidaiwa kupata kipigo kutoka kwa vijana waliojiita ‘Makamanda’ wa umoja wa vyama vya siasa vya upinzani ujulikanao kama Ukawa, baada ya baadhi yao kufika katika mkutano huo uliofanyika viwanja vya karibu na shule yao.
Baadhi ya viongozi wakuu wa umoja huo, akiwemo mwanasheria wa 
Chadema, Tundu Lissu, Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila 
(NCCR-Mageuzi) na Mbunge wa Arusha Mjini kwa tiketi ya Chadema, Godbless
 Lema, walishuhudia kitendo hicho, lakini cha kushangaza hawakuchukua 
hatua yoyote ya kuwazuia vijana hao kuwachapa watoto mijeledi kwa 
kisingizio kuwa hawakustahili kuwepo uwanjani hapo.
Hatua hiyo imekuja licha ya kuwa umoja huo ulikuwa unafanya mkutano 
wake katika eneo la shule ya Msingi Ngarenaro, uwanja ambao hutumika na 
shule za msingi za Ngarenaro na Mwangaza pamoja na shule ya Sekondari ya
 Ngarenaro.
Aidha, wanafunzi hao walikuwa na jukumu la kuotesha majani katika 
eneo hilo la shule. Katika mkutano huo, viongozi wa Ukawa walidai kuwa 
uwanja wa shule ya Ngarenaro ulikuwa umelimwa kwa trekta ili kuwazuia 
kufanya mkutano wao.
Hata hivyo, uongozi wa shule ulielezea kuwa katika kipindi cha mvua 
kama hiki, shule zote za manispaa huwa zinautumia msimu kuboresha 
mazingira kwa kuotesha majani, maua na miti kutokana na uwepo wa maji ya
 mvua.
Hata wale waliofika kwa ajili ya kusikiliza mkutano, pia walijikuta 
wakionja joto ya jiwe kutoka kwa ‘Makamanda’ hao. Kipigo cha wanafunzi 
pia kiliwakera wananchi wengi waliohudhuria mkutano huo na kulaani 
kitendo hicho.
Hata hivyo hakuna mtoto hata mmoja aliyeumia kutokana na sakata hilo,
 kwani walilazimika kukimbia kutoka uwanjani hapo kuepuka kipigo.
 RSS Feed
 Twitter

10:09 AM
MZM


0 comments:
Post a Comment