Friday, May 29, 2015

Rais mpya wa Nigeria Muhammadu Buhari leo (29.05.2015) anaapishwa rasmi ili kuanza kuingia madarakani Viongozi kutoka Afrika na sehemu nyingine za dunia wanahudhuria sherehe za kuapishwa Rais huyo mjini Abuja.
Rais mpya wa Nigeria Muhammadu Buhari Rais mpya wa Nigeria Muhammadu Buhari
Nigeria leo inakianza kipindi kipya cha historia.Wengi wanatathmini kuapishwa kwa Jenerali Buhari kuwa tukio muhimu kabisa katika historia ya Nigeria.
Kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi hiyo yenye watu karibu Milioni 178 mabadiliko ya uongozi yamefanyika baada ya uchaguzi wa amani.

Baadhi ya wachambuzi walifikiri kuwa Rais aliekuwamo madarakani hadi wakati wa uchaguzi,Goodluck Jonathan asingekubali kukabidhi mamlaka kwa Buhari kwa hiari yake.
Lakini Jonathan alikubali kushindwa na alimpongeza mshindi wa uchaguzi kwa moyo mkunjufu. Alichokifanya Jonathan kimezingatiwa kuwa ni ushindi wa demokrasia, siyo nchini Nigeria tu bali barani Afrika kote.
Mapambano dhidi ya ufisadi
Rais mpya amesema anadhamiria kupambana na ufisadi na kurejesha usalama nchini ambao kwa muda wa miaka kadhaa umekuwa unavurugwa na kundi la Waislamu wenye itikadi kali Boko Haram.
Rais anayeondoka wa Nigeria Goodluck Jonathan na rais mpya Muhammadu Buhari Rais anayeondoka wa Nigeria Goodluck Jonathan na rais mpya Muhammadu Buhari
Watu, nje na ndani ya Nigeria walishuhudia jinsi Buhari mwenye umri wa miaka 72 alivyoshinda uchaguzi kwa kupata asilimia 54 ya kura.
Hatahivyo pamoja na furaha zilizomo katika nyoyo za watu wanaomuunga mkono Buhari, wachunguzi wanasema Rais huyo mpya anapaswa kuonyesha uwezo katika harakati za kupambana na ufisadi.
Kipanga lazima akamate kuku
Mchambuzi mmoja, Tokede Williams amesema yule anaeitwa kipanga lazima awe na uwezo wa kukamata vifaranga. Watu nchini Nigeria wana duku duku kubwa juu ya ufisadi unaofanyika hasa katika sekta ya mafuta inayoiingizia nchi fungu kubwa kabisa la fedha.
Buhari mwenyewe amesema serikali yake mpya haitayafanya makosa yaliyofanywa na serikali iliyotangulia. Nigeria inapoteza mabilioni ya fedha kila mwaka kutokana na wizi na ufisadi katika sekta ya mafuta. Lakini Rais mpya, Jenerali Buhari anatambulikana kuwa mtu mwenye nidhamu ya hali ya juu.
Kuapishwa Buhari leo ni habari za kufurahisha kwa watu katika mji wake wa uzawa wa Daura, kaskazini mwa Nigeria. Watu wa mji huo wana furaha kubwa ya kumshangilia Jenerali Buhari, Rais wao mpya.
Lakini Buhari mwenyewe amesema watu wa mji huo wasitumai kupata zawadi kutoka kwake na pia amewataka watu wa familia yake wajiepushe na mambo ya rushwa.
Viongozi kadhaa wa Afrika na kutoka kwingineko duniani wanahudhuria sherehe za kuapishwa Rais mpya wa Nigeria Muhammadu Buhari mjini Abuja leo.Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry pia anahudhuria sherehe hizo mjini Abuja.

0 comments: