Wajumbe wa CCM wakiwa katika mkutano mkuu. 
IDADI kubwa ya wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), waliojitokeza 
kuchukua fomu ya kuomba kuwania nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
 Tanzania, imetajwa kutoa ahueni kubwa kwa vikao vya uamuzi na hasa 
Kamati Kuu, katika kufanya mchujo wake.
 
Wakizungumza na gazeti hili kuhusu kuibuka kwa zaidi ya wanachama 30 
wa CCM kuwania nafasi hiyo kubwa nchini, wasomi wa fani ya Siasa na 
Utawala wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, wameelezea namna ambavyo hatua 
hiyo itakavyorahisisha kazi ya kumpata mgombea.
Mmoja wa wahadhiri wa fani ya siasa chuoni hapo, Dk Jingu John, 
amesema kujitokeza kwa wagombea wengi, kunatoa fursa nzuri kwa kuwa 
wangejitokeza wachache, Kamati ya Maadili na Usalama na Kamati Kuu ya 
CCM ingekuwa katika wakati mgumu kufanya mchujo.
“Katika mazingira ya sasa tunaweza kusema kwa kufuata vigezo na 
kanuni zao, wanaweza kupata wagombea wazuri kuliko wangejitokeza 
wagombea kama wawili au watatu, ni kama wamepunguziwa kazi,” alisema Dk 
Jingu.
Msimamo wa JK Mhadhiri mwingine, Dk Benson Bana, alisema msimamo wa 
Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete wa kutokuwa na mgombea, umetoa 
matumaini zaidi ya kutoonesha upendeleo wakati wa kufanya mchujo.
“Chama sasa kinapaswa kudhihirisha kuwa kina uongozi imara, 
Mwenyekiti anatakiwa ahakikishe kanuni na taratibu zinazingatiwa… kama 
alivyowahi kusema urais hauna ubia, tunatarajia hata uenyekiti wake 
hauna ubia,” alisema Dk Bana.
Dk Bana alisema hatua ya Kikwete kutokuwa na upande wowote, imeonesha
 namna alivyokomaa kisiasa ndio maana mpaka sasa hajaonesha upande 
alioko na hata wagombea wanatarajia haki itatendeka.
Mwanzoni mwa wiki hii Rais Kikwete alipozungumza na Watanzania 
wanaoishi nchini Uholanzi, alikiri kuwa baadhi ya watangaza nia wamekuwa
 wakiomba ridhaa yake, ambapo yeye hakuna aliyemkatisha tamaa badala 
yake amemtakia kila la heri aliyejiona ana ubavu wa kutaka kumrithi 
baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Rais Kikwete katika hilo, alisema ana imani na chama anachokiongoza, 
kuwa kitafanya chaguo sahihi la mgombea wa urais atakayepeperusha vyema 
bendera ya CCM katika mchakato wa kumpata Rais wa Awamu ya Tano wa 
Tanzania baadaye mwaka huu.
” Huu ni mwaka wa uchaguzi, kuna mengi yanayoendelea, hasa mchakato 
wa kuwania urais… huko CCM mpaka leo (Jumatatu iliyopita) watu 15 
walishachukua fomu, na wengine zaidi ya 15 ama wametangaza nia au 
wanakusudia kufanya hivyo.
“Ndiyo demokrasia ndani ya CCM, lakini niwahakikishie acheni waumane,
 lakini mimi binafsi sina chaguo langu. Chama ndicho kitakachoamua na 
ninaamini kitatupatia kiongozi sahihi kwa saizi na hadhi ya CCM na huyu 
atatuvusha mpaka Ikulu. “Jana (Jumapili iliyopita), kuna mtu alinitumia 
ujumbe akisema anakusudia kutia nia hivyo nimpe baraka zangu…nikamwambia
 `Good luck’ (Kila la heri), sasa kama alitafsiri ndiyo tayari mambo 
safi, aah…sijui bwana, ila mimi sina mgombea.
“Nasisitiza chama chetu ni makini na kitatupatia mgombea makini. 
Mwenyezi Mungu atuepushie mbali ili tusipate kiongozi atakayeipeleka 
nchi pabaya,” alisema na kuwataka Watanzania wanaoishi nchini Uholanzi 
kutokuwa na hofu juu ya mchakato huo ndani ya CCM. CCM kumeguka?
Akizungumzia hofu ya watu kuwa huenda baadhi ya wagombea watakaokatwa
 wangeweza kutoka katika chama hicho na kujiunga na vyama vya upinzani, 
Dk Bana alisema haoni mgombea hata mmoja aliyejitayarisha kuhamia 
upinzani na ikitokea, haoni namna mgombea huyo atakavyojijenga kisiasa.
Vikao vya mchujo Mchakato wa uchukuaji fomu za kuomba ridhaa ya CCM 
kuwania urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ule wa Zanzibar 
ulioanza Juni 3 mwaka huu, unatarajiwa kukamilika Julai 2 mwaka huu.
Baada ya kuchukua fomu, kila mgombea ametakiwa kuzunguka mikoa 15 
nchi nzima, mitatu lazima iwe ya Zanzibar kusaka wadhamini 450, wastani 
wa wadhamini wasiopungua 30 kila mkoa, hatua ambayo imekuwa ikiendelea 
na kugonganisha wagombea katika mikoa mbalimbali nchini.
Kwa upande wa nafasi ya urais wa Zanzibar, ambayo mpaka jana hakukuwa
 na mgombea hata mmoja aliyejitokeza kuwania nafasi hiyo, mwanachama 
atakayechukua fomu, atatakiwa kutafuta wadhamini 250 kutoka mikoa mitatu
 ya Unguja na Pemba.
Baada ya kazi ya kupata wadhamini kukamilika, vikao mbalimbali vya 
uchujaji wa majina ya wagombea vinatarajiwa kuanza, vikitanguliwa na 
kikao cha Kamati ya Usalama na Maadili, kitakachokutana Julai 8, mwaka 
huu.
Kikao hicho kinatarajiwa kuandaa mapendekezo, yatakayosomwa na 
kujadiliwa na kikao cha Kamati Kuu kitakachokutana Julai 9, ambacho 
ndicho kinachoelezewa na wasomi kuwa kitakuwa na kazi nyepesi ya kuchuja
 majina ya wagombea, ili wapatikane wasiozidi watano watakaopelekwa kwa 
mchujo zaidi katika kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM.
Kikao cha Nec kinachotarajiwa kukutana Julai 10 mwaka huu, kitachuja 
majina hayo zaidi na kutoka na majina matatu, yatakayopelekwa katika 
Mkutano Mkuu utakaofanyika kwa siku mbili za Julai 12 na Julai 13 mwaka 
huu, ambapo pamoja na mambo mengine, mkutano huo ndio utakayemtoa 
mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa CCM na mgombea urais
 wa Zanzibar kwa tiketi ya chama hicho.
Wagombea Wanachama na vigogo waliokwisha kuchukua fomu kuwania nafasi
 hiyo kubwa kitaifa ni pamoja na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, 
Mathias Chikawe, Naibu Waziri wa Mawasiliano Sayansi na Teknolojia, 
January Makamba, Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja, mkazi wa Musoma 
mkoani Mara, Boniface Ndengo, mkulima kutoka kijiji cha Mjimtala wilaya 
ya Kasulu mkoani Kigoma, Eldefonce Bilohe na kada wa siku nyingi wa 
chama hicho, Dk Hassy Kitine.
Wengine ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, 
Bernard Membe, Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, 
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (Nimri), 
Dk Mwele Malecela na Mbunge wa Nzega, Dk Hamis Kingwangalla.
Pia yupo Balozi Amina Salum Ally, Waziri Mkuu wa zamani, Edward 
Lowassa, Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, Waziri wa Kilimo na 
Chakula, Steven Wassira, Waziri Mkuu wa zamani, Frederick Sumaye, Makamu
 wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal na Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli.
Wengine ni Balozi Ally Karume, Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina, Waziri
 wa Nchi Ofisi ya Rais Kazi Maalumu, Profesa Mark Mwandosya, Mtumishi wa
 CCM Idara ya Siasa na Uhusiano wa Tanzania, Amos Siyantemi na Waziri wa
 Uchukuzi, Samuel Sitta.
Pia yupo Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Wakili Mwandamizi Mahakama Kuu 
Tanzania, Godwin Mwapango, na makada wengine wa CCM, Peter Nyalile na 
Leonce Mulenda.
Wengine aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter 
Muhongo, Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk Titus Kamani, Mbunge
 wa Afrika Mashariki, Makongoro Nyerere, Balozi Agustino Mahiga, Mbunge 
wa zamani wa Iringa Mjini, Monica Mbega na kada wa CCM kutoka mkoani 
Tanga, Dk Mzamini Kalokola.