Thursday, June 25, 2015

 
 Makamu wa rais Burundi anaaminika kuwa ametorokea Ubeljiji 
Moja kati ya makamu wa rais wa Burundi ametoroka nchini humo baada ya kutangaza kuwa anapinga hatua ya rais wa nchi hiyo Pierre Nkurunziza kuwania muhula wa tatu.
Makamu wa pili wa Rais wa Burundi Gervais Rufikiri amekimbia baada ya kuiambia runinga ya France24 kuwa muhula huo wa tatu unakiuka sheria na katiba ya taifa hilo.

null
 Rais Nkurunziza alitibua mzozo baada ya kutangaza kuwania muhula wa tatu
Rais Nkurunziza alitibua mzozo baada ya kutangaza kuwania muhula wa tatu
Msemaji wa serikali hata hivyo amekanusha madai hayo na kusema kuwa bwana Rufikiri amesafiri nje kwa ziara rasmi ya kikazi.
Bwana Rufikiri amesema amekimbilia usalama wake akidai kuwa maisha yake yamo hatarini.
Msemaji huyo wa serikali amesema iwapo bwana Rufikiri ametoroka Burundi ni kwa maslahi yake mwenyewe wala hakuna yeyote aliyemtishia maisha yake.
null
 Umoja wa mataifa unaendelea na jaribio la kuwapatanisha mahasimu Burundi
Kutoroka kwake kunafwatia kutoroka kwa makamishna wa tume huru ya uchaguzi na jaji mmoja wa mahakama ya kikatiba.
Burundi imekumbwa na mzozo wa kisiasa tangu rais Nkurunziza atangaze hamu ya kuwania muhula wake wa tatu uongozini.
Wapinzani wake wanasema kuwa muhula huo wa tatu unakiuka katiba ya taifa.
null
 Uchaguzi nchini humo umeratibiwa kufanyika Julai tarehe 15
Kwa upande wake rais Nkurunziza anashikilia kukutu kuwa kulingana na makubaliano ya kusitisha vita ya Arusha, muhula wa kwanza aliochaguliwa na viongozi na wajumbe waliowakilisha majimbo hakuchaguliwa na umma kama inavyoelezewa na katiba ya nchi hiyo.
Kufikia sasa makundi ya upinzani yamekuwa yakiandaa maandamano katika barabara za Burundi wakimshiniza rais huyo achie ngazi.
Makundi ya kuteteza haki za kibinafsi yanasema kuwa hadi kufikia sasa watu 70 wameaga dunia katika makabiliano baina ya polisi wa kupambana na fujo na waandamanaji.
Zaidi ya watu wengine 500 wamejeruhiwa katika kipindi hicho cha miezi miwili iliyopita.
null
Zaidi ya watu laki moja wametoroka nchini humo wakihofia fujo 
Aidha zaidi ya watu laki moja wametorokea mataifa jirani kuepuka makabiliano na wengine kwa sababu ya hofu.
Mwezi uliopita jaribio la kumpindua madarakani bwana Nkurunziza lilitibuka.
Rais aliahirisha uchaguzi mkuu hadi tarehe 15 julai kufuatia shinikizo la viongozi wa kanda ya Afrika Mashariki na kati.
Umoja wa mataifa unaendelea na jitihada za kuleta uwiano baina ya serikali na makundi ya upinzani.
Burundi imesema itafanya mazungumzo na wapinzani baada ya uchaguzi wa wabunge na madiwani, utakaofanyika Jumatatu ijayo.
Taarifa hii imekuja baada ya serikali kususia mazungumzo ya amani kati yake na wapinzani yanayosimamiwa na Umoja wa Mataifa, na kusisitiza kuwa uchaguzi utafanyika licha ya wapinzani na shinikizo la kimataifa.

0 comments: